Tarehe 17 Septemba miaka 32
iliyopita, Mafalanja wa Lebanon wakishirikiana na askari wa utawala
haramu wa Israel walifanya mauaji makubwa katika kambi za wakimbizi wa
Kipalestina huko Sabra na Shatila nchini Lebanon. Mwezi Juni mwaka 1982
askari 150,000 wa utawala haramu wa Israel waliishambulia ardhi ya
Lebanon na baada ya kuwalazimisha wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi wa
Palestina (PLO) kuondoka Beirut na kuukalia mji huo kwa mabavu. Menachem
Begin Waziri Mkuu wa wakati huo wa Israel na Ariel Sharon Waziri wa
Vita wa utawala huo, tarehe kama ya leo waliliamuru jeshi la Israel
kuzizingira kambi za Sabra na Shatila na kisha Mafalanja wa Lebanon
wakaanza kufanya mauaji ya umati dhidi ya wakimbizi wa Kipalestina
waliokuwa katika katika kambi hizo. Wapalestina 3,300 waliuawa shahidi
katika mashambulio hayo.
Tarehe 26 Shahrivar miaka 34
iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, utawala wa zamani wa
Iraq ulifuta kwa upande mmoja makubaliano ya mipaka ya mwaka 1975
yaliyojulikana kwa jina la Mkataba wa Algeria kati yake na Iran. Siku
hiyo, Saddam Hussein kiongozi wa zamani wa Iraq aliuchana mkataba huo wa
Algeria mbele ya kamera za televisheni akiungwa mkono na madola ya
kibeberu katika. Siku kadhaa baadaye, Saddam Hussein alianzisha uvamizi
wa miaka minane dhidi ya ardhi ya Iran.
Na siku kama ya leo miaka 748
iliyopita alifariki dunia Ibn Nafis msomi na tabibu wa Kiislamu
aliyevumbua namna damu inavyozunguka kwenye mapafu. Alianza kujifunza
masomo ya dini ya Kiislamu akiwa katika mji alikozaliwa wa Damascus na
akafunzwa pia sayansi ya tiba na walimu mashuhuri wa zama hizo. Ibn
Nafis alipata maarifa makubwa baada ya kufanya utafiti wa kina. Mojawapo
ya vitabu mashuhuri vya Ibn Nafis ni kile alichokipa jina la" Muujaz al
Qanun (The Summary of Law) ambacho kinaelezea vyema namna damu ya mwili
inavyozunguka. Ibn Nafis alikuwa tayari amevumbua mzunguko huo wa damu
karne tatu kabla ya raia wa Ulaya, Miguel Serveto kubainisha kwa usahihi
kuhusu mzunguko huo wa damu katika mapafu. Al Shamil fi al Tibb ni
kitabu kingine cha msomi huyo wa Kiislamu kilichokusanya mjadala mpana
kuhusu mbinu za upasuaji.