18th Novemba 2015, Dar es salaam: Kampuni
ya Bia ya Serengeti (SBL) kupitia pombe yake kali ya Johnnie Walker imetangaza rasmi
udhamini wa mashindano ya gofu ya Waitara ambayo yanatarajiwa kuanza siku ya
jumamosi katika viwanja vya jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja
hivyo, Meneja Chapa wa pombe wa Kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) Bw. Shomari
Shija alisema kuwa udhamini wa mchezo huu wa gofu ni kuhakikisha kuwa unaweza
kuendelea na kusifika kama michezo mingine ikiwa pia kama moja ya sehemu ya
kurudisha fadhila kwa jamii inayotuzunguka.
“SBL inadhamini michuano hii kwa kipindi cha miaka
mitano sasa na itajikita hasa katika udhamini wa utoaji wa tuzo, vinywaji na
burudani katika kipindi chote cha mashindano”…alisema Bw. Shomari.
Naye katibu wa michuano hiyo ya gofu Kanali mstaafu
John Nyalusi aliishukuru SBL kwa kuendelea kusaidia maendeleo ya mchezo huo na
kuyaomba makampuni mengine kujitokeza na kuunga mkono jitihada hizo za kuinua
mchezo wa gofu nchini.
“SBL
imekuwa katika mstari wa mbele katika kuuendeleza mchezo wa gofu nchini. Ni
moja kati ya wadhamini wetu wa kudumu kwa sasa…hivyo tunawashukuru sana…
tunaomba makampuni mengine zaidi yajitokeze kuunga mkono jitihada hizi,”
alisema Kanali Nyalusi.
Aliongeza kuwa mashindano hayo yanatarajiwa
kufunguliwa na jaji mstaafu Ndugu Mark Bomani siku ya jumamosi saa nne asubuhi
na kuwa mpaka sasa mwitikio umekua mkubwa na tayari wachezaji 150 wameahidi
kushiriki mashindano hayo kutoka vilabu mbalimbali ikiwa ni pamoja na wenyeji
wa Lugalo Golf club, Dar es salaam Gymkhana club, Morogoro Gymkhana club,
Arusha n.k.
Mashindano ya gofu ya Mkuu wa Majeshi
mstaafu Jenerali George Waitara huandaliwa na kufanyika kila mwaka kwa
madhumuni ya kuenzi mchango wake wa kimichezo nchini kwa kuasisi uwanja wa gofu
wa Lugalo golf club. Uwanja wa gofu wa Lugalo ulianzishwa mwaka 2006 kwa
mchango mkubwa uliotolewa na Generali mstaafu George Waitara kipindi
alichokuwapo madarakani, pia kuendelezwa na Mkuu wa Majeshi aliyefuata na
aliyeko madarakani kwa sasa Generali Davis Mwamunyange.