Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), kina wagombea wawili wanaowania kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Madai
hayo mapya ya Profesa Lipumba yametolewa siku tatu baada ya kujiuzulu
uenyekiti CUF, akisema hiyo ni moja ya sababu za kuachia nafasi yake
kutokana na uamuzi uliofikiwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kuhusu mgombea urais.
Akizungumza
wakati akitangaza kujiuzulu wiki iliyopita, Profesa Lipumba alisema
dhamira yake ilikuwa inamsuta kwa kuwaingiza ndani ya Ukawa watu kutoka
CCM, waliokuwa wanapingana na maoni ya wananchi kuhusu rasimu ya Katiba
ya Jaji Warioba na kuwapa fursa ya kuwania urais.
Juzi
usiku katika mahojiano aliyoyafanya na Azam TV kutoka mafichoni
alikojificha ambako alisema anafanya utafiti, Profesa Lipumba alisema
kumpa nafasi waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa kuwania urais kupitia
Chadema ndani ya Ukawa, ni sawa na CCM kusimamisha wagombea wawili
(Lowassa- CCM B) na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli- CCM A)
Katika
mahojiano hayo ya simu, Profesa Lipumba ambaye wiki mbili zilizopita
alimpokea Lowassa akisema ni mtu safi na kwamba, ufisadi ndani ya CCM ni
mfumo alisema katika kujiuzulu kwake hakutumiwa na CCM kuparaganyisha
Ukawa, bali walikuwa tayari wameparaganyika.
“Ukweli
ni kwamba tumejiparaganyisha wenyewe ndani ya Ukawa. Kwa hiyo
Watanzania watakuwa na wanaCCM wawili wanaogombea urais wakati Ukawa
tulikuwa na wagombea watatu... mimi, Dk Willibrod Slaa, (Katibu Mkuu wa
Chadema) pamoja na Dk George Kahangwa (NCCR-Mageuzi) ambaye alikiri
kuwapo makubaliano hayo.
“Tulikutana nyumbani kwangu tukakubaliana Dk Slaa apeperushe bendera ya Ukawa, lakini tumewekwa kando,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema
yupo Rwanda kwa muda na anafanya utafiti kuona namna gani Tanzania
inaweza kujifunza mambo ya kiuchumi kutokana na nchi hiyo kupiga hatua
kubwa kiuchumi.
Pia alisisitiza kuwa hajahama nchi na kwamba wiki hii anatarajia kurejea nchini.
Agosti
6, mwaka huu Profesa Lipumba alijivua uenyekiti wa CUF wakati mkakati
wa vyama vya upinzani kushirikiana kushika dola ukiwa umeshika kasi.