HALI ni mbaya! Staa wa sinema za Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na mama
wa aliyekuwa nyota wa fani hiyo, Steven Kanumba, Flora Mtegoa wamefikia
pabaya baada ya mama huyo kumshushia Lulu maneno makali na ya shutuma,
Amani lina taarifa.
Habari zilizojiri ndani ya chumba cha habari cha gazeti hili zinadai
kuwa, mama Kanumba amemlalamikia Lulu kwamba, amemtupa na kumtenga
tofauti na zamani ambapo uhusiano wao ulikuwa kama wa mama na binti
yake.
“Jamani habari nzito kwa sasa ni mama Kanumba na Lulu. Mama Kanumba
anamshutumu Lulu kwa kumtenga. Anasema ni miezi mitano sasa Lulu
hajafika nyumbani kwake wala kuwasiliana naye kwa simu,” kilisema chanzo
kimoja.
Kikaendelea: “Hivi kesho (Jumanne iliyopita), ni Kanumba Day.
Imepangwa kufanyika Dar West (Dar), inawezekana Lulu asiende au Mama
Kanumba asiende. Lakini hata kama watakwenda na wakakutana, watachekeana
kwa jino pembe lakini uhusiano wao si mzuri jamani.”
MAMA KANUMBA ATAFUTWA
Ili kupata usahihi wa madai hayo, Amani
lilimsaka mama Kanumba kwa njia ya simu ambapo alipopatikana alikuwa na
haya ya kusema:“Lulu si Lulu yule jamani. Lulu sasa hivi amebadilika.
Awali aliniambia hatanitupa, lakini sivyo. Lulu siku hizi haji
kunisalimia wala hanipigii simu.”
ANACHOAMINI YEYE
“Imefika mahali nawaza kwamba, huenda alipenda
Kanumba aondoke ili yeye apate mafanikio makubwa aliyonayo sasa. Lulu
amenitenga, amenitenga, amenitenga!”
MANENO YA MAMA KANUMBA KABURINI KWA KANUMBA
Juzi, Jumanne, ambayo
ilikuwa siku ya kuadhimisha mwaka wa tatu tangu kifo cha staa huyo,
mama huyo alishiriki kwa kwenda kwenye Makaburi ya Kinondoni jijini Dar
kwa lengo la kusafisha kaburi la mtoto wake. Baada ya zoezi la kusafisha
kaburi kumalizika, mama Kanumba aliongea na Amani na kuyasema haya:
“Nasikitika sana namna ambavyo Lulu amekuwa tofauti na maneno yake ya
zamani kwamba atakuwa sambamba na mimi katika kuadhimisha kumbukumbu ya
Kanumba. Lakini leo kama hivi, hajatokea.
“Pia nasikitishwa na
kitendo cha kufanya bethidei ya mdogo wake jana (Jumatatu usiku) kule
Posta wakati anajua ndiyo usiku ambao Kanumba alifariki dunia.
“Mbaya zaidi, akiulizwa na watu kwa nini sasa hivi hayupo sambamba na
mimi kama zamani, anajibu majibu ambayo hayaeleweki. Kumbe maneno yake
ya zamani kwamba atakuwa sambamba na mimi yalikuwa ya usaliti.
“Kwa hiyo na mimi sasa nimeamua kubaki peke yangu kama nilivyo,
nitaendelea kumuenzi Kanumba mwanangu kwa sababu mimi ndiyo mama yake
kwa hiyo nalia peke yangu.”
LULU ALITOA AHADI YA UONGO
Katika mazungumzo yake, mama Kanumba
alikwenda mbali zaidi kwa kusema: “Kuna siku aliahidi kwamba atajengea
picha ya Kanumba ikiwa ndani ya kioo na kuiweka juu ya kaburi, hajafanya
hivyo. Nitafanya mwenyewe.“Labda amepuuza kwa vile anajiona anazidi
kukua kisanii, ni supastaa ndiyo maana anatoa ahadi za uongo.”
ALICHOKISEMA LULU SASA
Lulu alipotafutwa juzi ili kuzungumzia
malalamiko ya mama mkwe wake huyo, hakupatikana lakini wiki iliyopita
alizungumza na paparazi wetu kuhusu mtazamo wa maisha yake kwa jumla
ambapo alisema:“Mimi kwa sasa hivi nina mtazamo mwingine kabisa kuhusu
maisha. Kwanza sidhani kama nitamwaga machozi tena kuhusu Kanumba maana
nimelia sanasana.“Mtu ambaye naweza kumlilia ni mama yangu (Lucresia
Karugila) na mdogo wangu. Lakini si mtu mwingine. Kwa sasa naangalia
zaidi familia yangu.”
TUJIKUMBUSHE KIDOGO
Kanumba alifariki dunia Aprili 7, 2012 kwa
kuanguka katika mazingira yaliyodaiwa yalitokana na ugomvi kati yake na
Lulu. Tukio hilo lilitokea nyumbani kwa Kanumba, Sinza ya Vatcan, Dar.
Baada ya kifo hicho, Lulu alikamatwa na kuwekwa mahabusu ya Segerea jijini Dar na baadaye kuachiwa kwa dhamana.
Baada ya kutoka mahabusu, yeye na mama yake walimfuata mama Kanumba
na kuomba msamaha ambapo mama huyo aliupokea na kusema anamwona Lulu
kama mtoto wake na yote ya nyuma yamepita. Kuanzia hapo, Lulu na mama
Kanumba wamekuwa na ukaribu wa kindugu huku kila mwaka wakifanya
kumbukumbu ya Kanumba pamoja.
Katika kumbukumbu ya juzi, Lulu hakutokea na mama Kanumba alisema
hajapewa taarifa yoyote. Lulu alipotafutwa kwa simu ili kumsikia anasema
nini kuhusu kutotokea makaburini, hakuwa hewani!
Credit: Global Publishers