Diamond Platnumz ni msanii ambaye anazidi kuwa mkubwa nje ya mipaka ya Tanzania. Licha ya kuwa nyimbo zake karibu zote ni za Kiswahili, lakini haibadili ukweli kwamba moja ya kiungo kikubwa kati yake na wadau pamoja na wasanii wa kimataifa ni lugha ya kiingereza.
Mtoto wa Tandale hivi sasa anajivunia kuweza kukaa mbele ya kamera za vituo vikubwa vya TV na Radio za kimataifa na kufanyiwa mahojiano kwa lugha ya kiingereza mwanzo hadi mwisho, lakini yote hayo yamewezekana kutokana na jitihada zilizofanywa na mmoja wa wapenzi wake waliopita.
Lakini muimbaji huyo wa ‘Ntampata Wapi’ amesema kuwa sio Wema aliyemsaidia kumpiga brush kuongea lugha ya kiingereza kama ilivyokuwa ikidhaniwa na wengi.
“Kuna kitu watu hawakijui, watu wanafikiri eti Wema ndio alinifundisha mi kiingereza, lakini Penny ndio alinisaidia mi kiingereza wallah,” alisema Diamond kwenye mahojiano na Global TV.
“Aliniletea hadi mwalimu nyumbani, though nilikuwa namlipa mimi, lakini yeye ndio alinitafutia mwalimu wa kuja nyumbani, na ndio kiingereza hiki nachozungumza sasa hivi naamini kwa sababu ya msaada wa Penny ndio alinisaidia hadi nikafika hivi lakini watu wengine hawafahamu.”