Msanii kutoka TMK Wanaume Family, Amani James aka Mh Temba jana
amefikishwa katika mahakama ya mwanzo ya Temeke jijini Dar es salaam
akikabiliwa na mashitaka ya kutishia kuua kwa kisu kutokana na wivu wa
mapenzi.
Kwa mujibu wa Nipashe, Temba alipandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka yake mbele ya hakimu Claudia Frank wa mahakama hiyo.
Mheshimiwa Temba alifikishwa mahakani hapo mapema saa 3:00 asubuhi huku
akiwa amefungwa pingu chi ya ulinzi wa askari kanzu wa kituo cha Mkoa wa
Kipolisi Chang’ombe.
Aliwekwa chini ya ulinzi katika kituo cha mahabusu ya mahakama hiyo
kabla ya kusomewa mashitaka yake. Kesi hiyo imesajiliwa mahakamani hapo
kwa namba 371 chini ya kifungu cha 89 kidogo cha (2) (a) sura ya 16 ya
mwenendo wa sheria ya Makosa ya Jinai.
Akisomewa mashitaka na karani wa mahakama hiyo, Joyce Ngamesha, alidaiwa
kuwa Januari 28, mwaka huu, saa 1:00 jioni katika baa ya Scorpion
Iiliyopo Temeke jijini Dae es salaam, mshitakiwa alimtishia kumchoma
kisu Godrey Deogratius ama Sulla.
Mshitakiwa alikana mashitaka hayo na yupo nje kwa dhamana.
Hakimu Frank alisema kesi hiyo itasikiliza ushahidi March 11, mwaka
huu,. Kabla ya kufikishwa mahakamani hapo, Mshitakiwa alifikishwa katika
kituo cha polisi cha Chang’ombe akituhumiwa kutishia kumchoma kisu
mlalamikaji kwa madai ya kuwa na mahusiano wa kimapenzi na mke wa msanii
huyo.
Ilidaiwa kuwa mshitakiwa alimtishia kumchoma kisu mlalamikaji huku akijua ni kinyume na sheria.
Source:Nipashe