KWAKO mwanamuziki wa Injili na Bongo Fleva, Stara Thomas. Bila shaka ni
mzima wa afya na unaendelea na mishimishe zako maana najua una mambo
mengi, muziki wa kidunia na ule wa kiroho.
Binafsi
ni mzima. Naendelea na majukumu yangu kama kawaida. Nimekukumbuka kwa
barua leo maana ni muda mrefu hatujaonana. Sikulaumu maana mjini mipango
kama alivyoimba Mwanamuziki Ali Chocky wa Extra Bongo.
Dhumuni la barua hii kwanza kabisa ni kukupa pole kwa tukio lililotokea
juzikati maana suala la kukutwa na mwanaume mwingine tofauti na mumeo,
kila mmoja analijua uzito wake.
Hakuna anayeweza kulifurahia, nina imani hata wewe lilikufedhehesha sana
lakini hakukuwa na namna, ili mambo yaende lazima matukio kama hayo
yatokee, maisha yaendelee pia iwe fundisho kwa wengine.
Sambamba na kukupa pole, bado nina neno nataka kukupa. Sikufurahishwa na
tukio lile. Niwe mkweli kwamba kilichonifanya nisifurahi ni kwa sababu
wewe nakuheshimu.
Nilipoona umeingia katika skendo ile moyoni nikasema: “Vipi kwa wale ambao siwaheshimu, watakuwa wachafu kiasi gani?”
Sikia dada yangu, kitendo kile hakikuwa cha kiungwana. Heshima yako ni
kubwa sana katika jamii hivyo unapaswa kila unachokifanya uwe makini.
Mbali na kuwa mtu maarufu lakini wewe ni mama wa familia, tena watoto
wakubwa tu.
Kwa umri ulionao ukiingia katika skendo kama hiyo, ni aibu kwa wanao. Si
tu kwa wanao, kuna ishu ya waimbaji Injili wenzako ambao walikuwa
wanatambua mchango wako mkubwa.
Lazima waimbaji hao watakuwa wamesononeka sana. Utakuwa umewavunja
nguvu, hata wale ambao walikuwa wanapenda kazi zako, naamini pia utakuwa
umewakatisha tamaa.
Walikuwa wakitegemea wewe ambaye unawabadilisha tabia kupitia nyimbo
zako za Bongo Fleva na Injili uwe kioo cha tabia njema lakini badala
yake wanakuona umeangukia kwenye kashfa ya kukutwa na mchepuko.
Mbali na tukio hilo, baadhi ya matukio yako ya nyuma ambayo mengi
yalikuwa hayaripotiwi, yanaonesha kuna walakini kama kweli wewe ni kioo
cha jamii.
Unapaswa kujitathmini upya. Unapaswa kuangalia upya njia zako ili uweze
kuona sababu za kubadilika na kuwa mtu mwema. Naamini unaweza, hakuna
mwanadamu aliyemkamilifu.
Wengi tunakosea, tunaamka na kuanza upya safari. Safisha njia zako, kwa
imani tunaami ukitubu dhambi, Mungu pia anasamehe na hakika utakuwa
mpya.
Huna sababu ya kusononeka moyoni, chukulia kama changamoto ya maisha.
Wapo wengi wana matukio mazito kuliko hata hilo la kwako lakini
hayaonekani hadharani kwa sababu siyo watu maarufu.
Naamini utakuwa umenielewa, Mungu awe pamoja na wewe, nakutakia
mafanikio zaidi na uendelee kumtumikia Mungu wetu kwa nyimbo zako!
Kwa leo ni hayo tu!
Credit GPL