AMA kweli fedha mwanaharamu! Kama bado ulikuwa ukiamini
kwamba Beautiful Onyinye, Wema Isaac Sepetu anayependelea kuitwa Madam
ana mtonyo (fedha) kumzidi aliyekuwa shosti wake, mwigizaji Kajala
Masanja ‘Kay’, umekosea sana kwani upepo umegeuka, ungana na Ijumaa
Wikienda. Habari za ‘ufukunyuku’ zinadai kwamba, kwa utajiri alionao kwa
sasa, Kajala anaweza kudiriki kumwajiri Wema kama kisemavyo chanzo.
Mwigizaji wa filamu Bongo, Kajala Masanja ‘Kay’. TUJIUNGE NA CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo makini kilicho karibu na wote kwa maana ya
kutafuna pande zote, mwigizaji huyo ambaye enzi za ushosti wake na Wema
alikuwa akionekana kama kijakazi, sasa fedha imemtembelea kiasi cha
kutosha wakati mwenzake kwa bahati mbaya eti ‘anatembelea ringi’. Chanzo
kilisema kwamba Kajala kwa sasa ana maisha ya ‘kitonga’, amepanga
kwenye nyumba nzuri ya ghorofa, ana kampuni yake ya filamu (KAY
Entertainment), magari manne, anatembea na wapambe (walinzi) huku
akaunti yake benki ikiwa imetuna. “Kajala ameonesha jeuri ya fedha.
Ametoka katika nyumba ya kawaida sasa analala angani. Kwa taarifa yenu
amepanga ghorofa nzima maeneo ya Sinza-Madukani jijini Dar. “Yupo
vizuri, anamiliki ofisi kubwa ya kuzalisha sinema, magari mawili ya
ofisi pamoja na magari mawili ya kutembelea (Brevis na Harrier) na
anaishi katika nyumba anayolipa kodi kwa mwezi dola 2,000 (zaidi ya Sh.
milioni 3.2),” kilidai chanzo hicho na kudai kwamba si mbaya Kajala
akamkumbuka mwenzake hata kwa kumwajiri kwenye kampuni yake.
Pichani ni mjengo ambao Kajala Masanja amepanga.
KAJALA AMEHONGWA? Akizungumza na waandishi wetu, Kajala alisema
anamshukuru Mungu kwani fedha hizo amezizalisha kupitia kazi zake pamoja
na biashara mbalimbali alizokuwa akizifanya, hajahongwa na mtu yeyote.
“Sijahongwa na mtu yeyote, kila mtu ana akili zake katika kutafuta
fedha, nafanya biashara huku nikiigiza sinema zangu na Mungu amenijalia
mambo yanakwenda vizuri,” alisema Kajala. Kuhusu kumwajiri staa mwezake
huyo, Kajala hakutaka kulizungumzia hilo. WEMA HALI IPOJE?
Utafiti uliofanywa na Ijumaa Wikienda umebaini kwamba Wema aliyemlipia
Kajala Sh. milioni 13 asiende jela mwaka jana, ambaye kipindi kifupi
kilichopita alikuwa na kampuni ya kuzalisha sinema, wapambe, akaunti
iliyonona benki, magari ya kifahari ya kutembelea na samani nyingine,
nyingi zimepotea kama si kuyeyuka kabisa.
Gari la aina ya Toyota Brevis inayomilikiwa na Kajala.
Utafiti umeonesha Wema ambaye alikuwa akimiliki magari kadhaa likiwemo
la kufanyia kazi za sinema, kwa sasa amebakiwa na gari moja tu ambalo ni
Toyota Harrier. Kama hiyo haitoshi, ilidaiwa kuwa hata akaunti benki
haijanona na hata wapambe wa kutembea naye wameyeyuka. WEMA ATAFUTWA Ili
kutaka kujua anazungumziaje ‘challenge’ hiyo ya kudaiwa kuporomoka
kiuchumi, wanahabari wetu walimtafuta Wema kwa siku tatu mfululizo
lakini hakupatikana huku simu yake ikiita muda mrefu bila kupokelewa. SHOSTI WAKE
Akizungumza na waandishi wetu kwa sharti la kutoanika jina gazetini,
rafiki wa karibu wa Wema alikiri kuwa staa huyo mwenye nyota isiyochuja,
ameshuka kiuchumi tofauti na enzi zile ambazo walikuwa wakitanua katika
viunga mbalimbali na msururu wa watu huku Madam akisimamia shoo nzima
ya malipo. “Madam kwa sasa ameshuka kiuchumi kwani hatutanui mjini kama
ilivyokuwa zamani, yaani naamini anaweza kuajiriwa na Kajala ambaye
wakati ule alikuwa chini kwake,” alisema rafiki huyo.
Beautiful Onyinye, Wema Isaac Sepetu akitafakari jambo. KUMBUKUMBU YA JUZIKATI
Hivi karibuni, baadhi ya mashabiki wa Wema ambao wanajiita Team Wema,
walimuonya staa wao huyo wakidai ananyonywa na mpenzi wake, Nasibu Abdul
‘Diamond Platnumz’ ambaye pia amekuwa akimdhalilisha katika majukwaa
pindi anapofanya shoo zake. Walimtaka abadilike kwani yeye ndiye mwenye
nyota ya kung’aa lakini Diamond ananufaika yeye peke yake na muziki
wake. DIAMOND ALINENA Baada ya Diamond kushambuliwa na
Team Wema, naye alitoa majibu ambayo yalionesha dhahiri kwamba ndiyo
sababu inayomfanya Wema ashuke kisanaa na kiuchumi. “Kama kweli
mnampenda huyo msanii wenu (Wema) basi mngemshauri kwanza akaacha
kufanya starehe kuliko kuelekeza lawama kwangu, mimi kama mume, jukumu
langu ni kuhakikisha namwezesha kuanzisha biashara lakini jukumu la
kuendeleza ni la kwake, mnataka hata kuigiza nikamuigizie?,” alihoji
Diamond mtandaoni.


