Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetoa onyo pamoja na kutoza faini ya takribani Sh milioni 5 kwa kituo cha redio na televisheni cha Clouds, kwa kukiuka kanuni za utangazaji za mwaka 2005.
Wakielezea uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam, Kamati ya Maudhui ya mamlaka hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Margaret Munyagi ilisema kuwa ukiukwaji wa kanuni hizo ulifanywa kwa nyakati tofauti na vituo hivyo.
Alisema kwa upande wa kituo cha redio cha Clouds, kupitia kipindi chake cha ‘Njia Panda’ kilichorushwa hewani Juni 15 mwaka huu kati ya saa 8.00 mchana na saa 10.00 jioni kilikuwa na mada iliyohusu safari ya kuzimu ambapo maudhui yake yalijaa simulizi za kufikirika, za kishirikina na kichawi.
Aidha alisema kosa lingine kituo hicho hakikufuata kanuni za Utangazaji(maudhui) za mwaka 2005 zinazowataka kuwasilisha ratiba ya vipindi vyao kwa TCRA ili viidhinishwe na vilevile kuvichapisha katika gazeti kabla ya kurushwa hewani ambapo kipindi cha Njia Panda hakikuwasilishwa kwa ajili ya kuidhinishwa.
Wakati huo huo, kituo cha televisheni cha Clouds kilirusha kipindi cha ‘Bibi Bomba’ Mei 16 na Juni 6 mwaka huu kati ya saa 3.00 na saa 4.00 usiku ambacho kilikiuka kanuni za Utangazaji (maudhui) za mwaka 2005.
Alisema kipindi hicho kilidhalilisha mabibi hao walioshiriki pamoja na wanawake kwa ujumla kutokana na maswali ya aibu waliyokuwa wakiulizwa na waamuzi wa shindano hilo ambayo ni kinyume na kanuni hizo.
Aidha alisema kituo hicho kinatozwa faini ya Sh milioni moja na kutakiwa kuwasilisha TCRA mwongozo wa kuchuja na kusimamia maudhui yasiyofaa kabla ya kutangazwa.
TCRA imesema kama Kanuni za Utangazaji zitaendelea kukiukwa hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.